Anne Collier
Mwandishi na mtetezi wa masuala ya vijana Anne Collier
ameandika mijadala ya wazi kuhusu vijana na maudhui
dijitali tangu mwaka 1997. Yeye ni mwanzilishi na
mkurugenzi mtendaji wa shirika la kitaifa lisilolenga
faida linaloitwa The Net Safety Collaborative (TNSC),
ambalo mradi wake mkuu ni huduma za usaidizi kuhusu
mitandao ya kijamii mashuleni. Anne alihudumu katika
vikosi kazi vitatu vya kitaifa kuhusu usalama wa vijana na
Intaneti, ikiwa ni pamoja na kuwa mwenyekiti mwenza wa
Kikundi Kazi cha Teknolojia na Usalama wa Mtandaoni cha
utawala wa Obama pia katika Kikosi Kazi cha Kiufundi cha
Kitaifa Kuhusu Masuala ya Usalama wa Inteneti cha mwaka
2008. Hivi majuzi, alihudumu kwenye Kikosi Kazi cha
Taasisi ya Aspen cha mwaka 2013 hadi 2014 kilichohusu
Kujifunza na Intaneti.
Allison Briscoe-Smith
Allison Briscoe-Smith ni mwanasaikolojia wa kimatibabu wa
watoto aliyeidhinishwa. Ametumia kipindi chote cha kazi
yake katika taaluma na uandaaji wa mipango akiangazia
zaidi watoto na familia zinazokabiliwa na changamoto za
masuala yanayohusiana na haki za kimbari. Yeye ndiye mkuu
na mwanzilishi wa Soft River Consultation ambapo huwa
anatoa usaidizi, uandaaji wa mitaala, kuwezesha mashirika
yanayotaka kuondoa vikwazo vinavyowazuia watu kuhisi kuwa
wanastahiki.
Amanda Third
Profesa Amanda Third (PhD) ni Mtafiti Mwenza katika
Taasisi ya Utamaduni na Jamii; Mkurugenzi Msaidizi katika
Kituo cha Utafiti cha Vijana na Ustahimilivu katika Chuo
Kikuu cha Western Sydney; na Mshiriki wa Kitivo katika
Kituo cha Berkman Klein cha Intaneti na Jamii katika Chuo
Kikuu cha Harvard (2020-2023). Mtaalamu wa kimataifa
katika utafiti shirikishi unaolenga vijana, utafiti wa
Amanda unachunguza matumizi ya teknolojia kwa watoto na
vijana, ukilenga makundi yaliyotengwa na mbinu
zinazozingatia haki. Ameongoza miradi ya utafiti
inayolenga watoto kuelewa matumizi yao ya teknolojia
katika zama za kidijitali kwenye zaidi ya nchi 70,
akifanya kazi na watoto, vijana pamoja na washirika ambao
ni makampuni, serikali na mashirika yasiyo ya faida.
Ellen Selkie
Dkt. Selkie alitunukiwa shahada yake ya Utabibu na Uzamili
katika Afya ya Umma (MPH) kutoka Shule ya Tiba na Afya ya
Umma ya Chuo Kikuu cha Wisconsin ambapo kwa sasa yeye ni
Profesa Msaidizi katika kitengo cha Matibabu ya Watoto.
Kazi yake ya utabibu inahusisha malezi maalum yanayolenga
udhibiti wa makuzi ya vijana wadogo walio katika umri wa
balehe. Kama mtaalamu wa afya, Dkt. Selkie anatumai
atapunguza shughuli hasi za mitandao ya kijamii na
kuchochea shughuli chanya za matumizi ya mitandao ya
kijamii kwa vijana waliotengwa, hasa vijana walio katika
jamii za wachache kijinsia na utambuisho wa ngono.
Jessica Piotrowski
Dkt. Jessica Taylor Piotrowski ni Profesa katika Shule ya
Utafiti ya Mawasiliano ya Amsterdam (ASCoR) katika Chuo
Kikuu cha Amsterdam (UvA) ambapo yeye ni Mwenyekiti wa
Mpango wa Mawasiliano katika Jamii Ya Kidijitali. Utafiti
wa Dkt. Piotrowski unauliza jinsi tofauti za mtu binafsi,
kijamii na kitamaduni huathiri uchaguaji wa maudhui kwa
watoto, matumizi, na namna wanavyochanganua mambo na
athari zinazoweza kutokea, kwa kuzingatia hasa miktadha
inayounga mkono matumizi ya maudhui dijitali kwa vijana.
Justin Patchin
Profesa wa sheria za jinai katika Chuo Kikuu cha
Wisconsin-Eau Claire. Utafiti wa Justin Patchin
unachunguza uhusiano uliopo kati ya vijana wadogo na
teknolojia, kwa kuzingatia hasa uchokozi wa mtandaoni,
utumiaji wa mitandao ya kijamii na utumaji wa ujumbe wa
ngono. Yeye husafiri mara kwa mara ili kuwafundisha
wakufunzi, washauri, maafisa wa kutekeleza sheria, wazazi
na vijana kuhusu jinsi ya kuzuia matumizi mabaya ya
teknolojia.
Kareem Edouard
Kareem Edouard ni Profesa Msaidizi wa Teknolojia za
Kujifunza katika Shule ya Elimu katika Chuo Kikuu cha
Drexel na mshauri wa maudhui wa The Ole Greens Group. Dkt.
Edouard alitunukiwa Ph.D. katika mpango wa Kujifunza
Sayansi na Teknolojia katika Shule ya Uzamivu ya Chuo
Kikuu cha Stanford. Eneo lake la utafiti limejikita kwenye
kuelewa uhusiano uliopo kati ya mbari na tamaduni na
ushiriki wa wanafunzi wenye asili ya Afrika katika masomo
ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi Sanaa na Hisabati
(STEAM). Kazi ya ushauri ya Dkt. Edouard imejikita kwenye
ubunifu na utayarishi wa maudhui unaosisitiza kuhusu
umuhimu wa utamaduni na ujumuishwaji pamoja na mikakati ya
kujifunza.
Mimi Ito
Mimi Ito ni mwanaanthropolojia wa kitamaduni wa utamaduni
wa kidijitali na mtetezi wa mafunzo yaliyounganishwa
ambayo yanazingatia vijana, vitu wanavyopenda, shughuli za
kujifanyia na za kijamii. Yeye ndiye mwanzilishi mwenza wa
Connected Camps, shirika la faida ambalo hutoa fursa za
ubunifu za mtandaoni kwa watoto katika nyanja zote za
maisha. Utafiti wa miongo kadhaa kuhusu magwiji,
wachezaji, mashabiki, wanaharakati na wasanii umemshawishi
Ito kwamba watoto hujifunza vyema zaidi wanapofuatilia
mambo wanayovutiwa nayo na watu wanaowahamasisha.
Sameer Hinduja
Dkt. Sameer Hinduja anatambulika kimataifa kwa kazi yake
kubwa kuhusu uchokozi wa mtandaoni na matumizi salama ya
mitandao ya kijamii. Ameandika vitabu saba na utafiti wake
umetajwa zaidi ya mara 20,000 katika nyanja mbalimbali.
Dkt. Hinduja mara kwa mara hutoa ufafanuzi wa kitaalamu
kwa vyombo vya habari pia hufunza wanafunzi, wakufunzi,
wazazi, wataalamu wa afya ya akili na wanateknolojia njia
bora za kukuza matumizi chanya ya teknolojia.
Sarah M. Coyne
Dkt. Sarah M. Coyne ni Profesa wa masuala ya Ustawi wa
Binadamu kwenye Shule ya Maisha ya Familia katika Chuo
Kikuu cha Brigham Young. Mara kwa mara, yeye huzungumza na
familia na vijana kuhusu utumiaji wa mbinu na majukwaa ya
mawasiliano kwa njia bora. Alipokea shahada ya kwanza ya
Sayansi ya Saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Jimbo la Utah
na Shahada yake ya Uzamifu ya Saikolojia kutoka Chuo Kikuu
cha Central Lancashire jijini Preston, Uingereza. Masuala
anayoyatafiti yanahusisha mbinu na majukwaa ya
mawasiliano, ugomvi, jinsia, afya ya akili na ukuaji wa
watoto. Dkt. Coyne ana zaidi ya machapisho 200 kuhusu mada
hizi na nyinginezo. Ana watoto watano na anaishi Utah.
Sun Sun Lim
Sun Sun Lim ni Profesa wa Mawasiliano na Teknolojia katika
Chuo Kikuu cha Usimamizi cha Singapoo. Ameandika kwa upana
kuhusu matumizi ya vyombo vya habari na familia, ikiwa ni
pamoja na kitabu cha Malezi Yaliyopitiliza: Kulea Watoto
katika Zama za Kidijitali (Oxford University Press, 2020)
na Mawasiliano kwa njia ya Vifaa vya Mkononi na Familia
(springer, 2016). Anahudumu katika Baraza la Ufahamu
kuhusu Vyombo vya Habari na kuanzia mwaka 2018 hadi 2020
alikuwa Mbunge Aliyeteuliwa kwenye Bunge la Singapoo
ambapo alitetea haki za kidijitali kwa watoto na matumizi
yanayofaa ya AI na ufikiaji wa data.
Thiago Tavares
Thiago Tavares ni mwanzilishi na rais wa SaferNet, Kituo
cha Intaneti Salama cha Brazili ambacho kimedumu kwa miaka
18. SaferNet ndiyo shirika la kwanza kabisa lisilo la
kiserikali (NGO) nchini Brazili kuanzisha mbinu ya
kushirikisha wadau mbalimbali kulinda watoto na kukuza
uelewa wa haki za binadamu katika mazingira dijitali.
Tangu mwaka 2005 SaferNet imekuwa ikisimamia Nambari ya
Simu ya Huduma za Usaidizi ya Kitaifa na Kituo cha
Usaidizi na Uhamasishaji Elimu ya Usalama Mtandaoni cha
Brazili. Katika kipindi cha miaka 15 iliyopita kazi zake
kuhusu usalama wa watoto, usalama wa kidijitali na
udhibiti wa matumizi ya intaneti zimewasilishwa katika
zaidi ya nchi 30, yakiwemo matoleo tisa ya UN IGF.
Yalda T. Uhls
Yalda T. Uhls ni mwanasayansi wa utafiti anayetambulika
kimataifa aliyeshinda tuzo, profesa msaidizi wa chuo kikuu
cha UCLA na mwandishi wa kitabu cha Media Moms &
Digital Dads: A Fact not Fear Approach to Parenting in the
Digital Age. Yeye ndiye mkurugenzi mwanzilishi wa The
Center for Scholars & Storytellers, shirika la utafiti
katika chuo cha UCLA, ambalo linashughulikia kuondoa
utofauti uliopo kati ya utafiti wa sayansi ya jamii na
utayarishaji wa maudhui ili kusaidia uandaaji wa simulizi
zenye uhalisia na zinazojumuisha vijana. Ujuzi wa Dkt.
Uhls kuhusu jinsi ambavyo maudhui ya vyombo vya habari
yanavyotayarishwa na sayansi ya jinsi ambavyo maudhui
huathiri watoto hudhihirisha mtazamo wake wa kipekee.