Ni sera zipi zinashughulikia maudhui yasiyofaa?
Maudhui yoyote yaliyobuniwa kuchochea vurugu au kuleta chuki dhidi ya vikundi fulani vya watu yanakiuka sera yetu dhidi ya matamshi ya chuki. Pia, maudhui yanayotangaza au kusifu ugaidi yanakiuka sera yetu dhidi ya mashirika katili. Tunaondoa maudhui haya yakiripotiwa kwetu.
YouTube hushughulikia vipi maudhui ambayo hayakiuki sera lakini yanaweza kuchukuliwa kuwa hatari?
Wakati mwingine, kuna maudhui yanayokaribia kukiuka sera lakini hayakiuki. Yanafahamika kama maudhui yanayokaribia kukiuka sera. Mifumo yetu ya kutoa mapendekezo husaidia kudhibiti kuenea kwa maudhui yanayokaribia kukiuka sera na kwa sababu ya hili, kumekuwepo na kupunguka kwa zaidi ya asilimia 70 kwa muda wa kutazama maudhui haya yanayotoka kwenye mapendekezo ya jumla nchini Marekani.
YouTube inafanya nini hasa ili kuzuia maudhui yanayohimiza ugaidi au itikadi hatari?
Maudhui yanayotangaza au kusifu mashirika ya kigaidi na mengine ya uhalifu hayaruhusiwi kwenye YouTube. YouTube ina mifumo ya kiotomatiki ambayo husaidia katika utambuzi wa maudhui yanayokiuka sera zetu, ikiwa ni pamoja na sera yetu dhidi ya Mashirika Katili. Baada ya kutambua maudhui ambayo huenda yanakiuka sera, uhakiki unaofanywa na binadamu huthibitisha iwapo yanakiuka sera zetu. Kama maudhui yanakiuka sera, huondolewa na hutumiwa kufunza mashine zetu ili kutambua vizuri baadaye. Teknolojia ya mashine kujifunza sasa hutusaidia kuondoa maudhui hatari kabla hayajatazamwa zaidi. Kati ya Oktoba na Desemba 2019, takribani asilimia 90 ya video zilizopakiwa ambazo ziliondolewa kwa kukiuka sera yetu ya Itikadi Hatari, ziliondolewa kabla ya kutazamwa mara 10.
Jumuiya ya YouTube pia hutusaidia kutambua maudhui haya. Tumeweka chaguo la “yanaendeleza ugaidi” chini ya kila video kwenye YouTube, ambalo watumiaji wanaweza kuchagua wanaporipoti maudhui. Pia, tunashirikiana na wataalamu wa masuala ya itikadi hatari kupitia Mpango wa Wapigaripoti wa Kuaminika. Timu hukagua ripoti kwa makini kila wakati.
Sisi pia ni wanachama waanzilishi wa Global Internet Forum to Counter Terrorism (GIFCT), ambapo tunashirikiana na kampuni nyingine za teknolojia ili kuzuia maudhui ya ugaidi kwenye wavuti huku tukitoa mafunzo na nyenzo nyingine kwa kampuni ndogo zilizo na changamoto kama hizo.