Ni sera zipi zipo ili kupambana dhidi ya taarifa zisizo kweli kwenye YouTube?
Sera kadhaa katika Mwongozo wetu wa Jumuiya zinashughulikia moja kwa moja taarifa zisizo kweli.
Sera dhidi ya Maelezo ya Kimatibabu Yasiyo Kweli kuhusu COVID-19 hairuhusu maudhui yanayoeneza maelezo ya kimatibabu yasiyo kweli yanayokinzana na maelezo ya matibabu kuhusu COVID-19 kutoka kwa mamlaka za afya katika eneo au Shirika la Afya Duniani (WHO).
Mwongozo wetu dhidi ya tabia za udanganyifu unajumuisha sera thabiti dhidi ya watumiaji wanaojiwakilisha kwa njia ya uongo au wanaojihusisha na tabia nyingine za udanganyifu. Hii inajumuisha matumizi ya udanganyifu ya maudhui ya hila (k.m. “wahusika bandia”) ambayo yanaweza kusababisha hatari kubwa. Tunajitahidi pia kulinda uchaguzi dhidi ya mashambulizi na kuathiriwa, ikiwa ni pamoja na kulenga kukabili shughuli za kuathiri siasa.
Pia, tuna sera dhidi ya uigaji. Akaunti zinazolenga kueneza taarifa zisizo kweli kwa kujiwakilisha kwa njia ya uongo kupitia uigaji zinakiuka sera zetu na zitaondolewa.
Na mwishowe, sera yetu dhidi ya matamshi ya chuki hairuhusu maudhui yanayopinga kuwepo kwa matukio makubwa ya vurugu yaliyorekodiwa.
Je, YouTube hushughulikia vipi maudhui yanayokaribia kukiuka sera na taarifa hatari zisizo kweli?
Maudhui yanayokaribia — lakini hayakiuki — Mwongozo wetu wa Jumuiya ni sehemu ya asilimia moja ya maudhui yanayotazamwa kwenye YouTube nchini Marekani. Mifumo yetu ya mapendekezo haipendekezi maudhui kama hayo kwenye YouTube, hali inayosaidia kupunguza kusambazwa kwa video au maudhui yanayokaribia kukiuka sera ambayo yanaweza kupotosha watumiaji kwa njia hatari.
YouTube hubaini vipi maudhui yanayochukuliwa kuwa taarifa hatari zisizo kweli?
Tumeweka mifumo thabiti ya kutusaidia kubaini taarifa hatari zisizo kweli kwenye video nyingi katika YouTube. Kama sehemu ya mchakato huu, tunaomba wataalamu na wakaguzi kubaini iwapo maudhui yanahimiza matumizi ya njama au taarifa zisizo sahihi. Wataalamu hawa wamepewa mafunzo kwa kutumia mwongozo wa umma na hutoa mchango mkuu katika ubora wa video. Kutokana na mchango wa wakaguzi hawa, tunatumia mifumo ya mashine kujifunza iliyofanyiwa majaribio bora ili kubuni miundo inayotengeneza mapendekezo. Miundo hii husaidia kukagua maelfu ya saa za video kila siku ili kupata na kupunguza kuenezwa kwa taarifa hatari zisizo kweli.
YouTube hutoa vipi maelezo bora zaidi kwa watumiaji?
Kwa maudhui ambapo usahihi na kuaminika ni muhimu, ikiwa ni pamoja na habari, siasa, matibabu na maelezo ya kisayansi, tunatumia mifumo ya mashine kujifunza inayoipa kipaumbele taarifa kutoka vyanzo vya kuaminika katika mapendekezo na matokeo ya utafutaji.
Kwa aina fulani za maudhui ambayo huenda yana taarifa zisizo kweli mtandaoni, tuna vidirisha vya taarifa vinavyotoa taarifa za ziada kutoka vyanzo vingine vya kuaminika pamoja na video hizo ili kukupa muktadha zaidi wa kufanya maamuzi ya busara.
YouTube hutathmini vipi chanzo cha kuaminika?
Tunatumia ishara kadhaa ili kubaini kuaminika, ikiwa ni pamoja na hoja kutoka huduma za Tafuta na Google na Google News kama vile ufaafu na upya wa maudhui, pia ubora wa chanzo, ili kubaini maudhui unayoona katika mifumo yetu rasmi ya habari. Pia, tunatumia wakadiriaji na wataalamu wa nje ili kutoa maoni na mwongozo muhimu kuhusu usahihi wa video.
Taarifa zisizo kweli zinatofautiana vipi na taarifa za kupotosha?
Ni muhimu kuzingatia mtayarishi wa maudhui, pamoja na nia yake, kuamua iwapo maudhui hayo ni taarifa za kupotosha au taarifa zisizo kweli. Mtu akichapisha maelezo ya uongo, basi ni taarifa zisizo kweli. Iwapo mtu anajaribu kimakusudi kudanganya au kupotosha watu kwa kutumia kasi, kiwango na teknolojia za intaneti, basi tunabaini hali hii kuwa taarifa za kupotosha. Kwa kuwa taarifa za kupotosha ni sehemu ndogo ya taarifa zisizo kweli, tunatumia taarifa zisizo kweli kama hoja ya msingi kurejelea hali zote kwenye tovuti hii.